Na Anugrah Kumar




MAOFISA wa serikali nchini Marekani, wamekamata aina mbalimbali za nyoka wapatao 50 waliokuwa wakihifadhiwa katika Kanisa la Tabernacle Church of God la  LaFollette, Tenn., na Mchungaji Andrew Hamblin, ambaye amejizolea umaarufu mkubwa kupitia kipindi chake cha “Wokovu wa Nyoka” kinachorushwa katika kituo cha televisheni cha National Geographic, anakabiliwa na kesi ya kukutwa na wanyama hatari kwa binadamu.

     Mchungaji Hamblin akiwa ameshika nyoka 'albino' wakati wa ibada kanisani
 "Mimi sitadanganya. Wameuliza kama (nyoka) walikuwa nyumbani kwangu, nimesema hapana, lakini walipouliza kama wako kanisani, niliwaambia ndiyo,” Mchungaji Humblin ameuambia mtandao wa WBIR.com.
Hamblin, ambaye kwa mara ya kwanza alionekana katika kipindi hicho kinachojulikana kwa kimombo kama  "Snake Salvation," mapema mwezi Septemba, anaamini kuwa kanisa lake limelengwa na ‘kufuatwafuatwa’.   "Makanisa mengi siku hizi yanafichaficha mambo. Mimi sina cha kuficha."
Kushikilia majoka, kama ambavyo Mchungaji Hamblin amekuwa akifanya katika ibada imepigwa marufuku katika eneo la Tennessee tangu mwaka 1947, na mchungaji huyo anatuhumiwa kukutwa na mnyamna hatari wa daraja la kwanza, kwa mujibu waWBIR. Alitarajiwa kupandishwa katika mahakama ya Campbell County leo Ijumaa Novemba 15.
Kitendo cha kufanya ibada kwa kutumia nyoka katika maeneo kadhaa nchini Marekani imekuwa jambo la kawaida katika vikundi kadhaa vya Kipentekoste vyenye wafuasi wapatao 1000 hivi. Hawa huamini kuwa wameagizwa na Yesu Kristo katika Marko 16:15-18 na hasa mistari ya 17 na 18 katika Biblia ya King James, kushika nyoka.
Imeripotiwa kuwa Hamblin amewahi kung’atwa na nyoka wakati wa ibada kiasi cha mara tatu, lakini anadai kuwa kitendo cha kupandishwa kwake kortini ni kuingilia uhuru wa kuabudu.
"Sitajali sana kutokana na kuchukuliwa kwa nyoka waliokuwa kanisani kwa sababu nina uwezo wa kupata nyoka wengine wengi tu,” Mchungaji Hamblin alisema. “ Kinachoniumiza ni kwamba, hapa sio sehemu ya biashara. Hapa sio nyumbani. Ingekuwa ni nyumbani au sehemu ya biashara, sawa, wangewachukua (nyoka). Lakini hapa ni sehemu ya kuabudu”.
Hamblin pia alisema anawalisha vizuri nyoka wale, na kuna mashine ya joto kwa ajili yao wakati wa baridi kali.
"Ninaamini katika nguvu za Mungu… Lakini, sasa ninakabiliwa na kifungo jela, ninakabiliwa na hali ambayo nitatenganishwa na mke wangu, watoto wangu.Ninakabiliwa na hali ya kutupwa nje ya kanisa langu kwa sababu tu nilienda porini kukamata nyoka na kuwaleta kanisani kwa ajili ya kufanya huduma kama inavyosema kwamba tutashika nyoka,” alisema Mchungaji Humblin.
Pamoja na hatua hiyo, Mchungaji Hamblin alisema kanisa lake litaendelea na huduma ya waumini kushika nyoka, hapo baadaye.
Kipindi cha televisheni cha "Snake Salvation" tangu kianze kurushwa hewani kimekuwa kikiwachanganya Wakristo na watu wengine kwa ujumla.

0 comments:

Post a Comment

 
Top