Johannesburg.Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela amefariki dunia jana nyumbani kwake, Mtaa wa Houghton, Johannesburg akiwa na umri wa miaka 95.

Mandela aliyeliongoza taifa hilo kuanzia mwaka 1994 hadi 1999, kwa muda mrefu alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya mapafu na takriban nusu mwaka. Madaktari walimruhusu kutoka hospitali alikokuwa amelazwa kwa muda wa miezi mitatu na kushauri aendelee kupata matibabu nyumbani kwake.


Tangu juzi, ilielezwa kwamba kulikuwa na pilikapilika nyingi zilizoashiria kwamba pengine kungekuwa na tukio lisilo la kawaida.

Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma jana kwa majonzi makubwa alitangaza kifo cha Mandela na kusema kuwa kiongozi huyo mwenye historia ya pekee katika Bara la Afrika amepumzika kwa amani… “Baba Mandela amefariki na amepumzika kwa amani, taifa letu limempoteza mtu muhimu na wa pekee.”

Rais Zuma alitangaza msiba huo akiwa Ikulu, Pretoria Alhamisi saa 02:50 za Afrika Kusini (saa 03:50 usiku kwa saa za Tanzania) na kwamba kiongozi huyo alifariki akiwa amezungukwa na mke wake, Graça Machel pamoja na wanafamilia wengine.

Zuma alisema Mandela atafanyiwa mazishi ya kitaifa na kwamba kuanzia leo taifa hilo litakuwa kwenye maombolezo huku bendera zikipepea nusu mlingoti hadi hapo atakapozikwa.

Juzi, mtoto mkubwa wa Mandela, Makaziwe alisema afya ya baba yake ni mbaya na kwamba alikuwa amelala kwenye “kitanda cha mauti”.

Shirika la Habari la Afrika Kusini (SABC), lilimnukuu mtoto huyo wa Mandela akisema: “Baba bado yuko pamoja nasi, yuko mahututi, nadhani bado anatufundisha somo, somo la upendo na somo la uvumilivu.”
Mjukuu wa Mandela, Ndaba alinukuliwa na shirika hilo akisema: “Afya yake siyo nzuri sana, bado yuko na sisi, ingawa haendelei vizuri sana, bado yupo kitandani nyumbani.”

Dunia yamlilia
Chama tawala cha Afrika Kusini (ANC) leo alfajiri, kilieleza kusikitishwa kwake na kifo cha muasisi huyo.
“Taifa letu limempoteza shujaa wa haki, usawa, amani na haki ambaye alikuwa tumaini la mamilioni wa watu,” alisema Katibu Mkuu wa ANC, Gwede Mantashe.

Ugonjwa wake
Juni 8, mwaka huu hali ya Mandela ilibadilika ghafla na kulazwa katika Hospitali ya Med-Clinic, Pretoria kwa zaidi ya miezi mitatu, kisha kurejeshwa nyumbani kwake Johannesburg, Septemba mwaka huu ambako alikuwa akiendelea na matibabu hayo hadi mauti yalipomkuta.

Kulazwa kwake katika Hospitali ya Magojwa ya Moyo, Med-Clinic, kulizua taharuki na wasiwasi mkubwa miongozi mwa wananchi wa Afrika Kusini huku baadhi yao wakiweka wazi kwamba walikuwa wakisubiri habari mbaya kuhusu shujaa wao huyo.

Baadhi yao walikuwa wamekata tamaa na walipofika nje ya hospitali hiyo, walishindwa kujizua na kumwaga machozi. Kishindo cha ugonjwa wa Mandela kilionekana katika eneo la hospitali ya Medclinic, katika makazi yake Mtaa wa Houghton, Barabara ya Laan 12, Johannesburg na makazi yake ya zamani eneo la Soweto.

Maeneo hayo yalikuwa kwenye harakati zisizokoma kwani watu kwa mamia walikuwa wakifika kumtakia heri wakiwa wamebeba mabango, kadi, mishumaa na maua, huku wengine wakifika katika makundi wakiimba na kufanya sala.

Wapo walioifananisha hali iliyopo nje ya kuta za Medclinic na Houghton na ukuta uliokuwa umezunguka jela alikokuwa amefungwa katika Kisiwa cha Robben kwa miaka 18 kati ya 27 aliyokaa humo ikiwa ni adhabu aliyopewa na Makaburu kwa kupinga utawala wao wa kibaguzi.

Hata hivyo, matumaini yao yalirejea baada ya taifa hilo kuungana na naye katika maadhimisho yake ya miaka 95 wakati mwenyewe akiwa bado mahututi kitandani.

Mgogoro wa familia
Wakati Mandela akiendelea kuugua na hali yake ikielezwa kuwa ni mbaya, familia yake iliingia katika mogogoro mkubwa uliotafsiriwa na baadhi ya watu kwamba ni “kuwania madaraka” ikiwa kiongozi huyo angefariki dunia.

Familia hiyo ilifikisha suala hilo katika Mahakama ambayo ilitatua mgogoro wa ni wapi atakakozikwa na kuamua kwamba kiongozi huyo atazikwa Qunu uamuzi ambao uliacha ufa na uhasama mkubwa katika familia ya kiongozi huyo.

Wasemavyo kuhusu Mandela
Muda mfupi baada ya Mandela kufariki dunia, Rais wa Marekani Barack Obama alisema kuwa kiongozi huyo wa zamani wa Afrika Kusini, “Ni kama Malaika, leo amerudi nyumbani.”

Rais Obama alisema kuwa, yeye alikuwa ni miongoni mwa milioni ya watu waliovutiwa na Mandela.
“Kwa sasa tushukuru kwa ajili ya maisha aliyoishi Mandela, haitakuwa rahisi tena kuwapata watu wa aina ya Mandela, kwa hiyo ni jukumu letu kuendeleza yale aliyoyatenda, kutoa maamuzi ya upendo badala ya chuki, kuachana na tofauti zetu na kuishi maisha ya kujitolea,” alisema Obama.

Akizungumzia kifo hicho Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron alisema dunia imepoteza nuru, “Nasikitika kuona bendera zikipepea nusu mlingoni kutokana na kifo cha Mandela, alikuwa kiongozi wa Afrika Kusini na pia alikuwa shujaa wa miaka yote.”

Cameron ambaye aliandika ujumbe huo katika mtandao wa Twotter aliongeza, “Hakika mwanga uliokuwa ukiangaza dunia umezimika, namuona Mandela kama shujaa na kiongozi aliyefanya mambo makubwa kwa nchi yake na mataifa mengine, alikuwa mpenda amani.”

Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton, alisema, “kamwe siwezi kumsahau rafiki yangu Mandela.”

0 comments:

Post a Comment

 
Top