Na
Nestory Ngwega, Tanga
KATIKA hali isiyo ya
kawaida kutokea kwenye mikutano ya injili,watumishi wa mhubiri mwenye jina
kubwa nchini, Mchungaji Josephat Gwajima
wamemshambulia kwa kipigo kikali mwanafunzi wa chuo cha uandishi wa habari
ambaye pia mshirika wa Kanisa la Assemblies of God (TAG), jijini Tanga, Elias Mokiwa kwa kudaiwa kutenda kosa la kupiga
picha misukule inayodaiwa kurudishwa kupitia maombi ya huduma hiyo.
Tukio hilo
lililowashangaza watu wengi, wakiwemo
wasio Wakristo, lilitokea Jumapili Desemba Mosi, mwaka huu kwenye viwanja vya
Tangamano wakati mhubiri Gwajima (pichani) akiwa anaendelea na mahubiri yake ya kuwaita
misukule "njoooooo" akisisitiza kuwa kwa kuwaita vile misukule
wangetoka waliko na kwenda mkutanoni pale.
Kupigwa kwa kijana
huyo ambaye ni mwanafunzi wa chuo cha uandishi wa habari cha Royal kilichoko
jijini hapa, kulitokana na kitendo chake cha kupiga picha mama mmoja aliyedaiwa
kuwa ni msukule, ambaye alikuwa ameanguka mbele madhabahuni.
Elias aliwaambia
waandishi wa habari kuwa, baada ya kukamatwa akipiga picha, alichukuliwa na
kupelekwa nyuma ya jukwaa wakamvua mkanda ambao ulitumika kumfunga mikono yake
yote miwili kwa nyuma na kisha kumpa kipigo kama mwizi.
"Nilishambuliwa
kwa mateke ngumi na magongo..kwakweli najisikia maumivu sana. Tangu saa 12 jioni
waliponikamata waliniachia saa mbli usiku nikiwa nyuma ya jukwaa mahali ambapo
watu wengi walikuwa hawaoni tukio hilo isipookuwa mwanachuo mwenzangu mmoja
anayeitwa Veronica Mboto ndiye aliyeshuhudia na kutoa taarifa iliyopekea baadaye
kuokolea kutoka eneo hilo nililoliona kama kuzimu."alisema.
Kamanda wa Polisi mkoa
wa Tanga, Constatine Massawe alipoulizwa kuhusu tukio hilo alisema kuwa yuko safarini.
Hata hivyo, alisema kuwa kama kweli itathibitika watuhumiwa watachukuliwa hatua
kama wahalifu wengine. Alimwambia mwandishi wa habari hizi kuwasiliana na mkuu
wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa Tanga (RCO), Aziz Kimata.
Akizungumzia tukio
hilo, Kimata alisema kuwa watachukua hatua baada ya upelelezi wa awali
kukamilika.
Mchungaji Gwajima
ambaye ni kiongozi mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima hakuweza kupatikana
kuzungumzia tukio hilo, hata waandishi walipojaribu kukutana naye walinzi wake
waliwazuia. Hata simu yake ya mkononi pamoja na za wasaidizi wake wa karibu
zilikuwa hazipatikani mwandishi wa habari hizi alipopiga.
Baadhi ya wakristo
waliohojiwa na walionekana kushangazwa na tukio hilo, wakieleza kuwa haijawahi kutokea kwa wahudumu wa mkutano wa
injili kupiga watu kama ilivyotokea.
"Sisi wakristo
ikitokea miujiza kwenye mkutano wa injili tunawaita waandishi wa habari waje
watangaze kwani huo ni ushuhuda na watu wengine wajue kuwa Mungu wetu anaweza.
..sasa hawa wenzetu wanadai kufufua misukule ambao ni muujiza mkubwa halafu
hawataki waandishi kuwapiga picha na kuwatangaza, tuna wasiwasi na miujiza hiyo
kama ni misukule ya kweli au feki' alisema mtumishi mmoja ambaye hakutaka jina
lake liandikwe.
0 comments:
Post a Comment