Na Doris Petro
KWAYA ya Chang’ombe Vijana (CVC), ambayo iko chini ya Kanisa
la Africa Inland Church Tanzania (AICT), Ushirika wa Chang’ombe jijini Dar es
Salaam Desemba 29, mwaka huu itaadhimisha miaka 25 tangu ianzishwe.
Mwenyekiti wa kwaya hiyo, Elias Msula amesema kuwa, siku
hiyo kutakuwa na ibada maalum ya shukrani ambayo itafanyika kuanzia saa mbili
asubuhi. Alisema ibada hiyo itatawaliwa na kusifu na kuabudu. Ametoa wito kwa
watu wote bila kujali madhehebu yao kuhudhuria ibada hiyo, ambayo pia
itahudhuriwa na kwaya mbalimbali.
Alizitaja baadhi ya kwaya hizo kuwa ni AIC Dar es Salaam
Kwaya, Ukombozi ya KKKT Msasani, AIC Shinyanga pamoja na kwaya wenyeji. Hata
hivyo, amesema tukio hilo litatanguliwa na semina ya uimbaji ambayo itafanyika
Jumamosi Desemba 28 kanisani hapo.
Alisema kuwa, katika semina hiyo waimbaji kutoka makanisa
mbalimbali pamoja na Wakristo wote wanaalikwa kuhudhuria semina hiyo ambapo
mada mbalimbali zitatolewa. Miongoni mwa mada zitakazotolewa kwa mujibu wa Msula
ni “Uimbaji kama sehemu ya ibada na Waimbaji kujitambua kama Watumishi.”
Alisema miongoni mwa watumishi wa Mungu watakaotoa mada katika semina hiyo ni
Mchungaji Daniel Mgogo wa Kanisa la Baptist Mbeya.
Msula alisema tukio hilo litaenda sanjari na kuzindua rasmi
programu ya ujenzi wa jengo la kitega uchumi cha kwaya hiyo katika eneo la
Mtoni Kijichi. Aidha, alisema watauza cd yenye mchanganyiko wa nyimbo zilizomo
katika matoleo 12 ya kwaya hiyo tangu ianzishwe.
Akizungumzia mafanikio ya kwaya hiyo katika kipindi cha
miaka 25, Msula alisema kuwa, kwaya hiyo imekua kiroho na kiidadi. Alisema
wakati kwaya inaanzishwa mwaka 1988 ilikuwa na wanakwaya 15 lakini sasa ina
wanakwaya 90.
Kuhusu kukua kiroho, Msula alisema kuwa, kwaya imekuwa na
maombi ya kufunga kila Alhamis ya mwisho wa mwezi pamoja na vipindi vya
kujifunza neno la Mungu kila kabla ya kufanya mazoezi.
“Yapo mengi sana. Kwa mfano kwa miaka mitano kati ya mwaka
2007 na 2012 tumeshirikiana na kanisa la
AIC Ipagala mjini Dodoma kulijenga na kulikuza kwa kufanya mikutano ya Injili
kila Agosti ya kila mwaka. Tulishuhudia nyumba kwa nyumba na kufanya maombezi.
Tulipoanza waumini walikuwa hawazidi 20 lakini sasa kwa neema ya Mungu wako
zaidi ya 200,” alisema na kuongeza:
“Mwaka 1999 kuelekea 2000 kwaya ya CVC tulifanya mikutano ya
uinjilisti huko Eldoret nchini Kenya na watu wengi walimwona Mungu. Pia
tumehusika na umisheni kwa kufanya injili katika eneo la Usandawi, ambalo ni
miongoni mwa maeneo hapa nchini ambayo yalikuwa hayajafikiwa kwa injili kwa
kiasi kikubwa. Kwa kipindi hicho pia tumeweza kuwa na mradi wa studio
inayojulikana kama CVC Studio ambayo imetoa ajira kwa wanakwaya watano.”
Mchoro wa jengo la kitega uchumi ambalo linatarajiwa kujengwa na CVC
Kwaya ya CVC imeendelea kuwa miongoni mwa kwaya zenye
kupendwa na idadi kubwa ya wapenzi wa nyimbo za injili hasa kutokana na nyimbo
za Gusa, Vunja, Usiku wa Manane, Mpinga Kristo na nyingine nyingi.
0 comments:
Post a Comment