KANISA LA UFUFUO NA UZIMA LAJITETEA KUPIGWA MTU MKUTANONI
Na Mwandishi Maalum
MASAA machache baada ya mtandao huu kurusha hewani habari inayodai kuwa, mtu mmoja amepigwa kufuatia kumpiga picha mwanamke mmoja aliyedaiwa kuwa msukule, ambaye alifika kuitikia wito wa kiongozi mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Mchungaji Josephat Gwajima ambaye katika mikutano yake amekuwa akidai kuwaita misukule watoke waliko ili wafanyiwe maombi, uongozi wa kanisa hilo umekanusha habari hiyo.
Mchungaji Gwajima akihubiri mkutano mkubwa wa Injili jijini Tanga, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kuifikia mikoa kadhaa nchini kwa injili, ambapo alianzia Arusha na kufuatiwa na Kilimanjaro kabla ya Tanga.
Jumapili iliyopita (Desemba 1, mwaka huu), Elias Mokiwa, mwanafunzi wa chuo cha uandishi wa habari cha Royal cha jijini Tanga, anadai alipigwa na watendakazi wa kanisa hilo alipompiga picha mwanamke huyo katika uwanja wa Tangamano, ambako kulikuwa na mkutano wa Injili uliohubiriwa na Gwajima. Tayari tukio hilo limeripotiwa katika kituo cha polisi.
Lakini katika ujumbe wa maneno uliotumwa na mmoja wa viongozi wa kanisa hilo, Mchungaji Bihagaze kwa mmiliki wa mtandao huu, kanisa hilo limedai hakuna mtu aliyepigwa isipokuwa kuna kijana mmoja ambaye alijaribu kukimbia na mkoba wa mama mmoja aliyeangushwa na mapepo, lakini akadhibitiwa na walinzi na si watendakazi.
“Wakati tukio hilo linatokea watendakazi walikuwa frontline (mstari wa mbele) kukemea mapepo. Tunao askari jamii 24, askari mgambo walinzi 6 na askari kanzu wawili na waliovalia wawili. Hao ndio waliomkamata na baadaye tukawasihi wamsamehe.
Kwamba watendakazi ndio waliompiga hicho kitu hakuna jamani. Uwanjani waandishi wengi wa habari wanakuwepo. Wapo wa DTV, Startv, Mwambao FM, Breeze Fm . Wapo waandishi wa kawaida wa magazeti. Na wote hao wanapitia information desk wanapewa beji maalum za media hivyo wanakuwa na access (fursa) ya kupanda kwenye jukwaa na sehemu nyingine bila kuzuiwa.
Mbali na waandishi kuna watu maelfu ambao wana simu za kisasa ambao wakati mkutano unaendelea utawaona wamenyosha mikono wakirekodi kila kitu wapendavyo. Sasa katika mazingira kama hayo mtu anaweza kusema amekosa fursa ya tarifa katika mkutano; basi huyo mtu lazima ama awe taahira au ana mapepo mazito mno,” alisema Mchungaji Bihagaze katika ujumbe wake kwa mtandao huu.
Mokiwa ambaye ni muumini wa Kanisa la TAG jijini Tanga aliwaambia waandishi wa habari kuwa, alikamatwa na baadaye kupata kipigo kikali kutoka kwa aliowataja kuwa ni watendakazi wa kanisa hilo baada ya kupiga picha ya ‘msukule’ ambayo aliamini ilikuwa ni muhimu kwa jamii kama habari picha.
Mwanafunzi huyo wa taaluma ya uandishi wa habari alisema kuwa, baada ya kukamatwa na kupigwa alishikiliwa kwa muda wa zaidi ya masaa mawili nyuma ya jukwaa ambako ilikuwa ni vigumu kwa watu wengine kugundua, hadi mwanafunzi mwenzake, Veronika Mboto alipombaini.
Veronika ambaye pia ni mwanafunzi wa fani ya uandishi wa habari katika chuo hicho cha Royal, wiki iliyopita aliuambia mtandao huu kuwa alishindwa kupata habari katika mkutano huo wa Injili baada ya kuambiwa na walinzi na watendakazi kuwa hairuhusiwi wala uongozi wa kanisa hauhitaji habari za mkutano huo ziandikwe. Alidai alionywa asionekane akichukua habari.
0 comments:
Post a Comment