Na Mwandishi Maalum
MCHUNGAJI mwenye mahubiri yenye utata mkubwa katika nchi ya Kenya, ambayo shirika la kimataifa la UNICEF limeiorodhesha miongoni mwa nchi 30 maskini zaidi duniani ambako zaidi ya asilimia 25 ya wananchi kipato chao ni chini ya dola moja ya Marekani kwa siku, amekuwa akiwatoza waumini zaidi ya dola kumi (sh 17,000/= za Kitanzania) ili awaambie kama wataingia mbinguni.


Taarifa zinasema kuwa, mchungaji huyo maarufu ambaye pia huendesha mahubiri yake kwa njia ya televisheni, Thomas Wahome wa kanisa la Helicopter of Christ Church, alianza kuwatoza wafuasi wake kiasi cha shilingi 1,000 za Kenya au zaidi ya dola 10 za Marekani ili awaambie kama majina yao yameandikwa katika Kitabu cha Uzima. Katika imani ya Kikristo Kitabu cha Uzima ni mahali ambapo Mungu huorodhesha majina ya watu wanaostahili kwenda mbinguni.

Wahome, ambaye wafuasi wake wanamwita nabii, amekuwa akidai kuwa amepewa uwezo maalum wa kuona kurasa za kitabu hicho.

"Nimeshtuka. Marafiki zangu wameniambia majina yao yamo katika Kitabu cha Uzima na mimi eti ninapaswa kwenda kuangaliziwa kama nitaruhusiwa na mimi kwenda Mbinguni,” Sheila Mbaya, mama mwenye ndoa na mtoto mmoja aliliambia jarida la “The Nairobian”.

Jarida hilo liliwasiliana na huduma ya Wahome ili kuthibitisha madai ya Mama Mbaya ambapo mwanamke aliyejitambulisha kuwa ni Mchungaji Salome alisema kuwa itagharimu shilingi za Kenya 1,100 kuangaliziwa jina katika Kitabu cha Uzima.

"Tuma fedha kwenye namba hii, 07XX032000 (namba imehifadhiwa) na uje kesho kwenye saa nne hivi asubuhi . Askofu (Wahome) atakuambia kama jina lako limeorodheshwa katika Kitabu cha Uzima,” alisema.
Hii sio mara ya kwanza kwa Wahome kuibuka na “ufunuo tata” mbele ya waumini wake wengi wakiwa wanaokabiliwa na umaskini mkubwa.


Mwaka jana, aliwaambia wafuasi wake kuwa wanaweza kupata uponyaji kwa kugusa tu nguo zake kama Yule mwanamke mwenye damu ilivyonenwa katika Marko 5:21-34. Hata hivyo, aliwaambia uponyaji kwa kugusa nguo yake ungepatikana kwa kulipa shilingi 1,200 za Kenya.

1 comments:

 
Top