Mchungaji Humblin akiwa ameshika nyoka Ibadani



Mhariri: Mtandao wa “Fungukasasa” hivi karibuni, ukinukuu vyanzo mbalimbali, uliweka hewani habari kuhusu wachungaji wawili nchini Marekani; Jamie Coots na Andrew Hamblin , ambao wamekuwa maarufu ghafla baada ya kuanza kurusha katika televisheni ya “National Geographic” kipindi kinachowaonesha wakimwabudu Mungu huku wakiwa wameshikilia nyoka kuthibitisha kuwa na imani juu ya Mungu.



Mfano wa kipindi hicho ni sawa na vile vinavyorushwa na watumishi mbalimbali hapa nchini, kama vile Nabii G. Malisa wa Mwanza ambaye hurusha kipindi kiitwacho “Saa ya Ukombozi” au Antony Lusekelo ambaye hurusha katika televisheni kipindi kijulikanacho kama “Tutashinda”. Wachungaji hao wa Marekani wao wamekiita kipindi chao kuwa ni “Snake Salvation”, yaani “Wokovu wa Nyoka”.

Wachungaji hao  wanadai wanatumia nyoka katika ibada ili kama ilivyoandikwa katika Marko 16:17-18. Andiko hilo linasema: “Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhulu kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.”

Waumini nao wakiwa wameshika Nyoka Ibadani

Ingawa katika habari hiyo iliyoonekana kusomwa na watu wengi katika mtandao wa “Fungukasasa” kwa mujibu wa mpangilio wa habari zilizosomwa na watu wengi “popular post”, lakini kwingineko duniani habari hiyo imeibua mjadala mkubwa, huku baadhi ya wasomaji wakionekana kukasirishwa na kitendo cha wachungaji hao.

Hapa nchini Mkuu wa chuo cha Biblia cha Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), Mchungaji Geofrey Nnyani ambaye alifanya mahojiano na “Fungukasasa” akiombwa maoni yake kabla ya habari hiyo kuwekwa hewani alisema kuwa, kinachofanywa na wachungaji hao ni “kuchakachua” Biblia.

Mchungaji  Nnyani alisema kuwa, Biblia ina kanuni zake katika kuitafsiri.

“Kama wanatafsiri hivyo, basi waje huku watuhamishie na Mlima Kilimanjaro si imeandikwa tutahamisha milima!”, alihoji Mchungaji Nnyani. Alisema yeye mwenyewe amekuwa akishangazwa na baadhi ya mafundisho ya watumishi mbalimbali wa hapa nchini, hasa kwenye televisheni, ambapo alisema kumekuwa na upotoshaji mkubwa wa  maandiko matakatifu.

Mmoja wa wachungaji  wa Marekani, Hamblin amefanya mahojiano na mwandishi wa habari hivi karibuni, na ifuatayo ni sehemu ya kwanza ya mahojiano hayo:

Mwandishi: Tafadhali, hebu tueleze kwa kifupi kuhusu safari yako ya kiimani, mfano ulivyoingia katika Ukristo hadi kuwa mchungaji, na kadhalika?



Mchungaji Hamblin: Nimekulia katika Kanisa la Free Will Baptist ambako hata sasa huwa ninaweza kwenda kusali na hata kuhubiri. Babu yangu ni mchungaji pale. Wazee wangu walinikuzia pale. Naendelea, nikiwa na muda, naenda pale kuhubiri na babu yangu amewahi kuja kanisani kwangu kuhubiri.

Niliokoka tangu nikiwa na miaka 15 lakini sikuweza kuishi maisha yampasayo Mkristo kwa uhakika. Nilimjua Yesu Kristo katika maisha yangu. Lakini nilipofikisha miaka 17 niliamua sasa ninaenda kumtumikia Mungu maisha yangu yote. Ni wakati huo nilianza kusikia kuhusu makanisa yanayotumia nyoka katika ibada zake. Katika kanisa latu tunanena kwa lugha,- hata katika kanisa la Free Will Baptist-tulinena kwa lugha, tuliimba kwa kushangilia, tuliamini katika ubatizo wa Roho Mtakatifu, ni kama tu inavyokuwa katika makanisa ya Kipentekoste, au yale ya church of God.

Sasa nilipoona watu wakishika nyoka, wakinena kwa lugha, wakibatizwa kwa roho mtakatifu, wakiimba na kucheza, nikaona hapakuwa na tofauti kubwa, hivyo nilitaka kujua kama hili la kutumia nyoka ni kiroho au la.

Ndio siku moja nikaenda kanisani kwa Mchungaji Jamie Coots. Nilipata habari za kanisa hilo nikajisemea ningepata wapi mtu wa kunipeleka huko-walinipeleka. Huko nilimwona Mchungaji Jamie akienda kuchukua  masanduku mawili wakati ibada ikiendelea. Nilivyoona hivyo nikahisi kuna kitu kikubwa zaidi kinaenda kutokea.

Baadaye nilijiunga katika kanisa hilo. Nilipiga gitaa, niliimba, na nilihubiri, lakini kamwe sikujihusisha na nyoka. Walinishikia nyoka wakanielekezea, lakini mimi nilisema hapana sijui kitu hicho. Niliendelea kusali. Lakini baada ya mwaka mmoja hivi siku moja niliona kwa mara ya kwanza katika maisha maisha halisi Mungu akianza kushughulika na mimi. Mungu aliniongoza kwenda kwenye sanduku lililohifadhi nyoka, wakati huo nilikuwa na miaka 18. Nilianza kuhisi upako wa roho mtakatifu kwa namna ambayo nilikuwa sijawahi kuihisi maishani mwangu. Nilianza kujisemea, Mungu ni wewe ndiye unanivuta huku…….niliomba na nilijiweka mbele za Mungu…..nilisema Mungu kama ni wewe unayenivuta huku….kulikuwa na sanduku lenye nyoka watatu wakubwa. Nazungumzia nyoka wenye urefu wa nchi 44-45. Nilijisemea Mungu kama ni wewe unanivuta huku-ninataka nimshike Yule nyoka mkubwa kuliko wote kwenye hili sanduku-nilisema, uruhusu Mchungaji Jamie awashike hao nyoka wote, nitajua ni wewe (Mungu) unayenivuta kufanya haya.

Sikufanya lolote zaidi ya kuomba kwamba Mchungaji Jamie awatoe nyoka wale. Kweli aliwashika. Kuona vile nilihisi upako wa ajabu unaniingia nilienda kwenye sanduku nikamshika nyoka-nilimshika kwa sekunde kama 30 hivi kisha nikamrudisha kwenye sanduku. Tangu pale niliendelea kuimarika.

Mwandishi: Kwanini ulikubali kushiriki katika kipindi cha “Wokovu wa nyoka”?

Mchungaji Humblin: Sababu pekee iliyonifanya nikubali kushiriki kwenye kipindi cha “Wokovu wa nyoka”  ilikuwa sio labda kuona watu Fulani  hawaingii katika ibada ya kushika nyoka, yaani niwavute kuja kwenye ibada hizo.Hilo halikuwa kusudi langu.

Kama watu wanavutiwa-sawa siwezi kusema kuvutiwa-nitasema wanaamini, yaani waanze kuamini, hilo ni jambo jema. Sababu iliyonifanya nishiriki katika kipindi cha “Wokovu wa nyoka”  ilikuwa ni kueneza Injili katika nchi yote, na hata duniani kote. Kuwaambia watu kwamba wanaweza kuokolewa. Sio waamini kama mimi, sio wavae kama mimi, sio washike nyoka kama mimi. Lakini kuwafanya waelewe kuwa damu ya Yesu bado inaokoa na Yeye ni halisi.

Nilifikiria-kuna wahubiri wengi kwenye tv-wainjilisti na wachungaji, wanahubiri hili na lile, na hilo ni jambo jema. Nilitaka tu kusema, unajua mimi ni kijana mdogo kabisa katika nchi hii. Sio lolote mbele za mwanadamu. Lakini kwa sababu ya damu ya Yesu, mimi nina thamani mbele za Mungu, na nilitaka kuonesha mwanga mbele ya wanadamu.

Lengo langu limefanikiwa. Kuna mamia ya watu ambao wananitumia ujumbe tofauti, mfano mchungaji tulikuwa hatuamini lakini baada ya kuangalia kipindi imetuongezea imani kwa Mungu, tumeangalia kipindi, tulikuwa hatuamini kama kuna Mungu, mchungaji sisi ni Wapentekoste tunapenda kujifunza zaidi kuhusu hilo (la kutumia nyoka ibadani) tunajisikia kama Mungu anasema na sisi kuhusu hilo.

Imenishangaza. Nilifikiri watu watatuelewa vibaya. Lakini huduma hii imekuwa na matokeo mazuri. Najua katika kila zuri kuna kinyume chake, lakini nimeona mazuri mengikuliko mabaya. Kama nilivyosema lengo langu ni kuona watu wakiokolewa. Sijali wanashika nyoka au …..wanaimba, wanacheza na kuvaa kama mimi, wanajiunga na kanisa la First Baptist au lipi. Kwangu la muhimu ni kuokoka kwao.

Mwandishi: Tafadhali niambie kwa kifupi kuhusu kanisa lako, lina waumini wangapi, limeanzishwa lini, na kadhalika. Pia, liko chini ya dhehebu gani na linafuata misingi ipi?

Mchungaji Humblin: Siku hizi washika nyoka kwenye ibada wanaitwa  ni watu wa Pentecostal Holliness. Kanisa langu linaitwa Tabernacle Church of God na lilijengwa mwaka 1994. Mtu aliyelijenga bado ndiye mmiliki na ninamtambua kama ndiye mwanzilishi. Tunachukulina naye vizuri sana. Ila yeye alikuwa hajawahi kushika nyoka. Halikuwa kanisa la washika nyoka hapo awali, lilikuwa kanisa la kawaida la Church of God. Hadi nilipokuja hapo kuwa mchungaji. Mwezi Novemba mwaka huu nitatimiza miaka miwili tangu niwe mchungaji hapo.

Aliyelianzisha alilifunga kutokana matatizo ya kiafya, aliugua magonjwa tofauti tofauti. Lakini tangu niwe hapa amekuwa akishika nyoka. Kanisa letu sio la kidhehebu. Sisi ni Wakristo. Dhehebu kwangu mimi ni kazi ya wanadamu. Ninamaanisha kwamba kama uko kwenye dhehebu hilo ni jambo la ajabu. Kama unasaidia dhehebu lako hiyo ni ajabu zaidi kwani ni vigumu kwenye dhehebu kukuta watu wenye utaratibu unaofuiatwa kwa dhati kabisa kwenye dhehebu.  Kanisa letu linafuata mafundisho ya Kipentekoste, Holiness na Church of God, lakini kimsingi sisi ni kanisa lisilo chini ya dhehebu lolote.

Mwandishi: Una waumini wangapi mpaka sasa?

Mchungaji Humblin: Krismas iliyopita tuliorodhesha waumini tukaona walifika kama mia na ishirini hivi. Ni vigumu kuwapata wote kwa wakati mmoja. Tulikuwa tunapata waumini 10 hadi 15 katika ibada moja, lakini siku hizi kanisa limekua. Tunapata watu sio chini ya 30 na sio zaidi ya 80 lakini kanisa linaendelea kukua. Kama kila aliyeguswa na kipindi, maana wameniandikia wakisema “mchungaji tunakuja”, basi tutakuwa na watu wengi sana pale, na tutalazimika kuondoa na kutafuta eneo jingine.

Mwandishi: Mara ngapi mnafanya ibada?

Mchungaji Humblin: Tuna ibada kila Ijumaa saa 1:30 asubuhi na kila Jumapili saa saba mchana, na kila Jumamosi ya kwanza ya kila mwezi saa moja asubuhi. Naliongea hili kila ninapofanya mahojiano na waandishi wa habari. Tunataka kila anayesoma mahojiano haya afahamu kuwa anakaribishwa sana. Haijalishi anatoka dhehebu gani au imani gani-tunawakaribisha sana  waje waabudu pamoja na sisi na wawe pamoja na sisi. Hawawezi kushika nyoka, hawawezi kuwa karibu na nyoka.  Sio katika kila ibada tunashika nyoka.

Mwandishi: Tukio gani baya limewahi kukutokea wewe au muumini wako wakati wa kushika nyoka?

Mchungaji Humblin: Hakuna tukio lolote kwa waumini. Bwana ametubariki sana na ametuwekea ulinzi. Hatujakutana na baya lolote. Kitu kibaya kwangu ni pale nilipong’atwa na nyoka. Sikuwa katika huduma ya kikanisa. Nilikuwa katika chumba cha nyoka na mimi mwenye ndiye nilizembea. Hapakuwa na upako mle. Ilikuwa sawa na mtu anayeng’atwa na nyoka akiwa porini. Nilizembea ndio maana nyoka Yule alining’ata na nilisikia maumivu makali.

Na kweli nilienda hospitali. Niliwaambia waumini kwanini nilienda hospitali.
Next
Newer Post
Previous
This is the last post.

0 comments:

Post a Comment

 
Top